KIAZI KIKUU NI ZAIDI YA CHAKULA, INATIBU!!!!

    Kiboko ya kisukari, `gono’, ukoma
  Hutibu  bawasiri, matatizo ya hedhi, moyo




Na James Zakayo

KIAZI kikuu au kwa kitaalamu, Dioscorea alata, sio maarufu sana miongoni mwa watu katika jamii, lakini umaarufu wake unaweza kutokana na kile kinachobainishwa na wataalamu kuwa pamoja na kwamba ni chakula, pia ni mmea dawa.
Ni mmea unaotambaa kwa msaada wa mti mithili ya mmea mwingine maarufu wa mpensheni, lakini tofauti yake ni kwamba  mizizi yake hunenepa na kutambaa chini ya ardhi kama ilivyo muhogo au viazi vitamu na mizizi hiyo huitwa viazi vikuu.
Dk. Raphael Nyampiga ni mtaalamu wa miti na mimea dawa kutoka kliniki ya miti na mimea dawa inayojulikana kama Atukuzwe ya Pugu Jijini Dar es Salam, anasema mmea huo huweza kuwa na urefu  wa zaidi ya mita moja na kwamba kiazi kimoja hufikia uzito wa hadi kilogramu 50 kulingana na eneo ulimopandwa.
Katika mahojiano na TABIBU hivi karibuni, Dk. Nyampiga anasema hata hivyo  misombo (compounds) zilizomo kwenye  kiazi husaidia kupambana na sumusumu mwilini hasa kwenye kongosho, shambulio la moyo, bawasiri na huondoa uzito uliopitiliza mwilini na kitambi.
“Tangu zamani kiazi kikuu kilifahamika kama tiba ya matatizo ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na tiba ya bawasiri. Hii ni kwa sababu kina wingi wa kamba lishe na misombo inayotibu ugonjwa huo,”alisema.
Faida zingine za kiafya za kiazi kikuu, Dk. Nyampiga anasema kuwa ni miongoni mwa vyakula vinavyosaidia  kusafisha damu na kuondoa vikwazo katika mishipa ya damu vinavyozuia damu kuzunguka mwili.
Pia kamba lishe hizo zina uwezo wa kurekebisha kiwango cha sukari mwilini, matatizo ya hedhi na kuweka sawa mfumo wa homoni za uzazi kwa mwanamke.
Husaidia  kuondoa  muingiliano wa homoni zinazovuruga mfumo wa hedhi na huongeza  kuzaliana kwa homoni inayochochea uzalishwaji wa mayai kwa mwanamke, alisema.
Kwa wasichana wanao karibia umri wa kuvunja ungo (kupevuka), wanashauriwa na mtaalamu huyo kula kwa wingi kiazi kikuu kwani  kinapoliwa katika umri huo husaidia zaidi kuweka sawa homoni zao katika mwili pindi watakapoanza mzunguko wa hedhi.
Kwa upande mwingine, tafiti za nje ya Tanzania kuhusu tiba inayotokana na kiazi kikuu, Dk. Kurian katika kitabu chake cha Healing Wonders of Plants anasema pamoja na kutibu maradhi yanayotajwa na Dk. Nyampiga, pia  hutibu ukoma.
Zaidi,  anaainisha katika utafiti wake kuwapo kwa virutubisho kadhaa kwenye kiazi kikuu kama vile protini, mafuta, wanga, sukari na kamba lishe. Pia vitamini vya thiamini, riboflavini, niazini na folate.
Virutubisho vingine  kwenye kiazi  kikuu ni madini ya magneziamu, kalisiamu, chuma, fosforasi, potaziamu, sodiamu, zinki,  kopa, seleniamu, manganizi, misombo  ya beta-karotini,  folikiloriki na pantotheniki ambavyo kuwapo kwake mwilini husaidia kupambana na maradhi hayo.
Pia hutibu ugonjwa wa zinaa aina ya kisonono maarufu kwa vijana wengi kama `gono’ ambao ni kifupisho cha neno la kitaalamu la gonorrhea, kabla haujakomaa mwilini.
“Ili kuweza kuondoa na kupunguza sumusumu na magonjwa katika mwili wa binadamu,  lazima tukubali na kuheshimu vyakula vya asili  na ambavyo havikusindikwa na kuchanganywa na kemikali,” alisema.


Nao, utafiti uliofanywa na ripoti yake kuchapishwa katika jarida la Philippine Journal of  Science , unaibainisha kuwa, kiazi kikuu ni chanzo cha vitamini B6, ambayo husambaratisha kemikali  hatari kama vile homocysteine.
Kemikali hiyo, huathiri mishipa ya damu na kuzuia damu kutofika sehemu zote za mwili hivyo kusababisha  tatizo la shambulio la moyo, sehemu ya utafiti huo imeonesha.

MATUMIZI:

Dk. Kurian anashauri kuwa ili kutibu magonjwa  hayo,   mhusika anatakiwa kukatakata kiazi kikuu vipande vidogo vidogo, kuvichemsha kwa muda wa dakika 20 hadi 30, kisha kula kwa kadri ya uwezo wake. Inashauriwa kula  mlo huo mara kwa mara.
“Ni muhimu  kunywa supu ya viazi vilivyopikwa wakati wa kula mlo huu kwani supu hiyo imebeba mchangnyiko wa virutumisho hivyo ,”alisisitiza.
Naye Dk. Nyampiga: “Kiazi kikuu kinaweza kumenywa na kukaushwa juani, kusagwa kama ilivyo muhogo. Mgonjwa wa kisukari au mhudumu  wake achanganye unga wa kiazi kikuu kiasi cha nusu kijiko kidogo na maji ya moto katika ujazo wa kikombe cha chai,  kisha kunywa kwa dozi ya kutwa mara mbili, kwa mfano asubuhi na jioni, ”alifafanua.

==============

Comments

Popular posts from this blog

faida ya pili pili manga mwilini katika kutibu magonjwa

UJI WA ULEZI HUIMARISHA KIWANGO CHA SUKARI KWENYE UBONGO