UJI WA ULEZI HUIMARISHA KIWANGO CHA SUKARI KWENYE UBONGO


Na James Zakayo
         WATU wengi katika jamii huamini na kutumia chai kama kifungua kinywa. Yamekuwa mazoezi enzi na enzi. Bahati mbaya sana ni kwamba watu wengi hufungua kinywa bila malengo.
Katika hali hiyo, Dk. Raphael Nyampiga wa kituo cha tiba lishe cha Atukuzwe chenye makao yake, Pugu nje kidogo ya Jijini la Dar es Salaam anasema ni muhimu jamii kutambua ni kifungua kinywa gani ni sahihi na kupata kiburudisho hicho kwa malengo.
Zaidi, mtaalamu huyo anasema katika kutambua usahihi na malengo ya kifungua kinywa ni muhimu pia kutambua umuhimu wa lishe bora, kunywa au kula kwa muda gani na kipi kiliwe na kwa  muda upi kulingana na aina hizo za chakula ikiwamo kifungua kinywa hasa uji wa ulezi.
Anasema uji wa ulezi ni miongoni mwa vyakula muhimu  katika afya ya binadamu, yafaa jamii kukitumia kwa wingi zaidi kama kifungua kinywa, kulingana sifa zake mwilini na virutubisho vilivyomo.
 “Unapokunywa uji wa ulezi asubuhi kama kifungua kinywa mara baada tu ya kutoka kitandani kabla ya kula kitu chochote huchukua nafasi kubwa sana ya kufanya siku yako kuwa bora zaidi katika majukumu yako ya siku nzima”alisema Dk. Nyampiga na kuendelea...
 “Kifungua kinywa hiki pia kinawawezesha  wanafunzi kufaulu vizuri mitihani yao na kupata alama za  juu kwa mitihani waliyofanya kabla ya mapumziko yao ya mchana…nguvu hizo zinazotokana na kifungua kinywa cha uji wa ulezi zimeimarisha kiwango chao cha sukari kwenye ubongo, na zimeimarisha uwezo wa kufikiri,  pia kuwa wasikivu.” alisema.
Pia alisema kuwa ndani ya uji wa ulezi kuna virutubisho muhimu vya kuifanya akili kufanya kazi ya kuwa na kumbukumbu na mwili kuwa na nguvu kubwa katika kumfanya mtoto awe na ari ya kujisomea ndio maana hata mama wajawazito wanashauriwa kunywa uji wa ulezi mara baada ya kujifungua ili kurudisha nguvu.
“Wakati wa miaka 70 tulikuwa tunashindia uji wa ulezi kutokana na virutubisho vilivyomo ndani yake kwa kuwa vilitupatia nguvu kubwa ya kuufanya mwili kuwa na nguvu ya ziada kwa muda mrefu , lakini kwa kuwa sasa  hivi watoto wetu wengi hawapewi uji wa ulezi asubuhi hivyo hawawezi kuwa na uvumilivu wa kushinda muda mrefu bila kula” alisema.
Kwa kuunga mkono hoja hizo naye Dk. Raymond Shirikisho kutoka KCMC alisema kuwa mwili wa binadamu unafanya kazi kama mashine hivyo kama kuna kifaa hakina mafuta muhimu na ya kutosha basi si rahisi msuguano kutokea ili mashine ifanye kazi, hivyo unywaji wa kifungua kinywa asubuhi na mapema unapoamka ni muhimu kwa afya ya akili.
“Unywaji wa uji wa ulezi ni muhimu pale unapoamka kwa kuwa unafungua akili ili iweze kufanya kazi katika  kiwango cha juu tofauti na wale wasiokunywa kifuangua kinywa cha aina yoyote”alisema Dk. Shirikisho.

Walitoa wito kwa jamii kurudi katika kula vyakula vya asili na kuachana na vyakula visivyo na tija katika mwili wa binadamu. “Wazazi wanaaswa kuwandalia watoto wao uji wa ulezi asubuhi na mapema kabla hawajatoka kwenda shuleni ili kuweza kufungua akili ya mtoto na kuwajengea uwezo mkubwa wa kufikiri,”alisema Nyampiga. 

Comments

Popular posts from this blog

faida ya pili pili manga mwilini katika kutibu magonjwa

KIAZI KIKUU NI ZAIDI YA CHAKULA, INATIBU!!!!